Polisi wamkamata waliyetengeneza video za utupu za Baobab
Sisti Herman
January 20, 2025
Share :
Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limemkamata mtu mmoja ambaye alitengeneza picha chafu zisizo na maadili kuhusu wanafunzi wa shule ya Baobab iliyopo Bagamoyo mkoani humo, ambapo uchunguzi wa kitaalam ulisaidia kumfikia na kumkuta na picha hizo na kifaa cha kielektroniki ambacho alikuwa akitumia kusambaza picha hizo chafu.
Taarifa ya leo Januari 20, 2025 iliyotolewa na Ofisi ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani imeeleza kuwa mnamo Januari 3,2025 Jeshi hilo lilipokea taarifa kutoka kwa uongozi wa shule ya Baobaob iliyopo wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani ya kutengenezwa na kusambazwa katika mitandao ya kijamii picha mjongeo za utupu zenye maudhui machafu kimaadili lakini pia ni kinyume na sheria za nchi.
“Picha hizo chafu na zisizo za kimaadili, waliotengeneza waliunganisha na baadhi ya majengo ya shule ya Baobab ili kuuaminisha umma kuwa vitendo hivyo vinafanyika shuleni hapo Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linatoa onyo kwa watu wenye tabia kama hizo za kutengeneza na kusambaza picha kama hizo kwa malengo ya kuchafua wengine au taasisi kwani mkono wa sheria lazima utawafikia na hata kama hautawafikia mapema wataendelea kupata shida ya kujificha na kuacha kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo,” imeeleza taarifa hiyo