Polisi wawaua watekaji wakiwaokoa watoto Mwanza
Sisti Herman
February 9, 2025
Share :
Wanafunzi wawili wa Shule ya Blessing Model School waliotekwa Februari 5, 2025, jijini Mwanza wamepatikana wakiwa hai, huku watekaji wao wakipigwa risasi na kuuawa baada ya kujaribu kuwashambulia askari kwa silaha za jadi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa, amesema kuwa watoto hao walikutwa wakiwa wamefichwa katika nyumba namba 8, iliyopo Mtaa wa Nyabulogoya, Kata ya Nyegezi.
Aidha ameeleza kuwa operesheni ya kuwaokoa watoto hao ilifanyika baada ya polisi kupata taarifa za uwepo wa watekaji hao ndani ya nyumba hiyo. Ameeleza kuwa baada ya askari kuzingira eneo hilo na kutoa amri kwa watekaji kujisalimisha, watekaji hao walijitokeza wakiwa na mapanga na marungu, hali iliyosababisha polisi kutumia silaha za moto.
Watoto hao, Magreth Thobias Juma (8), mwanafunzi wa darasa la pili, na Geofrey Mwakalebela (5), mwanafunzi wa darasa la kwanza, walitekwa wakati dereva wa gari la shule alipopakia abiria asiyejulikana, ambaye baadaye alimshambulia dereva huyo na kutoweka na watoto wawili kati ya sita waliokuwemo kwenye gari hilo.
Taarifa za awali zilionyesha kuwa watekaji walikuwa wakitoa madai ya fedha kwa uongozi wa shule ili kuwaachia watoto hao huru. Kamanda Mutafungwa amesema uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini mtandao mzima wa uhalifu uliokuwa nyuma ya tukio hilo na kuhakikisha wahusika wote wanachukuliwa hatua za kisheria.