Polisi yapiga marufuku maandamano kwenye jiji la Nairobi
Eric Buyanza
July 18, 2024
Share :
Polisi nchini Kenya wamepiga marufuku maandamano katikati ya mji wa Nairobi na viunga vyake.
Hayo yamejiri huku Kenya ikiendelea kushuhudia maandamano ambayo yalianza tangu mwezi Juni, kupinga Mswada wa Fedha 2024.
‘’Nchi yetu imekuwa ikishuhudia hasara kubwa, watu wamejeruhiwa, kupoteza maisha, mali na biashara zimeharibiwa,’’ taarifa ya Polisi ilisema.
Iliendelea kusema kuwa imepokea taarifa kwamba baadhi ya makundi ya kihalifu yanapanga kutumia vibaya maandamano ya siku ya Alhamisi, Julai 18, 2024 kutekeleza mashambulizi na uhalifu.
"Kukosekana kwa uongozi katika maandamano yaliyopita kumefanya kuwa vigumu kuhakikisha itifaki za usalama zinafuatwa. Kwa sababu hiyo, hakuna maandamano yataruhusiwa katika eneo la kibiashara katikati ya mji wa Nairobi na viunga vyake ili kuhakikisha usalama wa raia," taarifa hiyo iliendelea kusema.
Raia waliombwa kuwa makini katika maeneo yenye watu wengi, kushirikiana na polisi na kutoa taarifa zozote ambazo zinaweza kusaidia kubaini uhalifu.