Polisi yawaonya wenye mpango wa kuhatarisha amani
Sisti Herman
May 25, 2025
Share :
Jeshi la Polisi nchini limewahakikishia wananchi kuwa lipo imara na linaendelea kuhakikisha linadhibiti vitendo vyote vya kihalifu kwa mujibu wa sheria, likisisitiza kuwa halitasita kuchukua hatua dhidi ya mtu au kikundi chochote kitakachojaribu kuvuruga amani ya nchi.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, CP Awadhi Juma Haji, wakati wa kuhitimisha mafunzo ya medani za kivita kwa wanafunzi wa kozi ya Uafisa na Mkaguzi Msaidizi wa Polisi katika kambi ya Polisi ya Mkomazi mkoani Tanga, leo Jumamosi Mei 24, 2025.
Kamishna Awadhi aliwataka wahitimu hao kutumia vyema mafunzo waliyoyapata katika maeneo watakayopangiwa, kwa lengo la kutatua changamoto mbalimbali, hususan zile zinazohusiana na uhalifu ndani ya jamii.
Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Dk Lazaro Mambosasa amesema kuwa askari hao wamejengewa uwezo katika maeneo mbalimbali, yakiwemo mbinu sahihi za kukabiliana na matishio ya kiusalama, ili kuhakikisha usalama wa wananchi unaendelea kudumishwa.