PSG Yarusha taulo kusaka saini ya Olise Madrid bado wanakomaa.
Joyce Shedrack
July 18, 2026
Share :
Mabingwa wa Ufaransa, Paris Saint-Germain (PSG), wanaripotiwa kujiondoa katika mbio za kumsajili nyota wa Bayern Munich, Michael Olise, kutokana na kutokuwa tayari kulipa ada inayokadiriwa kufikia euro milioni 200.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, PSG haitaki kuingia katika vita ya zabuni kwa mchezaji huyo, jambo ambalo limeiacha Real Madrid ikiwa mbele katika harakati za kuipata saini yake.

Inadaiwa kuwa Olise anatamani kuhamia Santiago Bernabéu baada ya kuwa na msimu bora nchini Ujerumani, ambapo alifunga mabao 22 na kutoa pasi 31 za mabao katika mashindano yote.
Ripoti zinaeleza kuwa rais wa Real Madrid, Florentino Pérez, anamwona Olise kama nyota wa kiwango cha "Galáctico" ambaye anaweza kuongeza makali ya safu ya ushambuliaji pamoja na Kylian Mbappé.
Aidha, inasemekana Olise tayari amezungumza na wachezaji wenzake wa timu ya taifa ya Ufaransa, Kylian Mbappé na Aurélien Tchouaméni, ili kupata maoni kuhusu maisha na mazingira ya kuchezea Real Madrid.
Kwa upande wa PSG, viongozi wa klabu hiyo wakiongozwa na mkurugenzi wa michezo Luis Campos na rais Nasser Al-Khelaifi, wanadaiwa kubadili mkakati wa usajili kwa kuelekeza nguvu zao katika kusaka vipaji vinavyochipukia badala ya kutumia fedha nyingi kwa nyota ambao thamani yao tayari imepanda.





