Punda wagongwa na gari,mizoga yatelekezwa barabarani
Eric Buyanza
October 21, 2026
Share :

Punda wawili wamefariki dunia baada ya kugongwa na gari lililokuwa likiendeshwa kwa mwendo kasi katika barabara kuu ya Arusha–Namanga, eneo la Engikaret, Wilaya ya Longido, mkoani Arusha, huku mizoga yao ikiachwa kando ya barabara kwa zaidi ya nusu siku bila kuondolewa.
Tukio hilo lilitokea Oktoba 16, mwaka huu, ambapo kwa mujibu wa mashuhuda, punda hao waligongwa na gari hilo usiku wa manane au alfajiri, kabla ya dereva kuondoka eneo la tukio.
Mbarwa Kivuyo, kutoka taasisi ya Kangai Foundation na mwanachama wa Chama cha Kitaifa cha INADES FTZ, alisema alishuhudia tukio hilo alipokuwa akisafiri kutoka Arusha kwenda Longido kuhudhuria kikao cha Kamati ya Wilaya ya Usimamizi wa Biashara ya Hewa Ukaa katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido.
Alisema kilichomsikitisha zaidi ni kukuta mizoga ya punda hao ikiwa bado kando ya barabara saa 8:00 mchana alipokuwa akirejea Arusha, hali iliyoibua maswali kuhusu hatua zilizochukuliwa na mamlaka husika kufuatia ajali hiyo.
NIPASHE





