Rais azua mjadala, ampa binti yake majukumu ya 'Mke wa Rais'
Eric Buyanza
March 15, 2024
Share :
Rais wa Pakistan Asif Ali Zardari amemtambulisha rasmi binti yake Aseefa Bhutto Zardari kama 'First Lady' wa nchi hiyo, wakati kikawaida hadhi ya 'First Lady' huwa inakwenda kwa mke wa Rais.
Kutangazwa kwa binti huyo wa miaka 31 kuwa mwenye hadhi ya mke wa Rais, kumezua minong'ono, mijadala na maswali mengi nchini Pakistani pamoja na duniani kwa ujumla.
Rais Zardari alikua 'mgane' baada ya mke wake aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani Benazir Bhutto kuuawa mwaka wa 2007.
Zardari hakuoa tena na nafasi ya mke wa rais ilibaki wazi katika kipindi chake cha kwanza cha uongozi kama rais kuanzia mwaka 2008 hadi 2013.
Zardari mwenye umri wa miaka 68 aliapishwa kuwa Rais wa 14 wa nchi hiyo siku ya Jumapili (Machi 10,2024) na amekuwa Rais wa kwanza kuchaguliwa mara mbili katika nafasi hiyo.
Wakati wa hafla yake ya kula kiapo katika Ikulu ya mjini Islamabad, Zardari aliandamana na binti yake Aseefa.