Rais Samia amuunga mkono RC Makonda kambi ya madaktari Arusha.
Joyce Shedrack
June 24, 2024
Share :
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amepiga simu mubashara na kuzungumza na wananchi wa Arusha waliohudhuria siku ya kwanza ya Kambi maalum ya Madaktari bingwa wanaotoa huduma za matibabu bure kwa wakazi wa Mkoa wa Arusha.
Rais Samia amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda na kamati yake kwa kuandaa kambi hiyo huku akiahidi kutoa ushirikiano kama kutakuwa na upungufu wowote utakaojitekeza muda wowote wa kambi hiyo.
" Serikali kuu itaangalia nini cha kuwekeza hapo ili kuunga mkono jitihada za mkoa ili wananchi wapate matibabu", Amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Dkt. Samia amewapa pole wananchi wote wenye kusumbuliwa na matatizo mbalimbali ya kiafya akiahidi kuendelea kuboresha huduma za afya ili kuhakikisha huduma za afya zinapatikana za uhakika na zenye kukidhi mahitaji ya wananchi.
Katika kambi hiyo madaktari bingwa na watoa huduma za afya zaidi ya 450 kutoka kwenye Hospitali na Taasisi takribani 40 za afya nchini Tanzania wanatarajiwa kutoa huduma za vipimo na matibabu bure kwa wakazi wa Mkoa wa Arusha kwa siku saba mfululizo kuanzia leo Juni 24, hadi juni 30,2024.