Rais Samia apeleka Bilioni 669 za barabara na madaraja mikoa ya Kusini.
Joyce Shedrack
May 27, 2025
Share :
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametangaza kuwa serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan itatumia kiasi cha shilingi bilioni 669 kwa ajili ya ujenzi wa barabara na madaraja katika mikoa ya Lindi na Mtwara kwa lengo la kuboresha usafiri na kuifungua mikoa hiyo kiuchumi.
Akizungumza mkoani Mtwara, Ulega alisema barabara na madaraja hayo yatajengwa kupitia barabara za Mtwara āMingoyo (Mnazi mmoja)-Masasi itakayogharimu kiasi cha shilingi bilioni 401 huku barabara nyingine ya Mtwara Tandahimba-Newala-Masasi itagharimu kiasi cha shilingi bilioni 268 hadi kukamilika kwake.
Waziri Ulega amewaambia wananchi wa Mtwara kwamba kiasi hicho kikubwa cha fedha katika ujenzi wa miundombinu hiyo unaonyesha dhamira ya dhati aliyonayo Rais Samia kwa wananchi wa mikoa ya Kusini na lengo kubwa ni kuhakikisha inafunguka kiuchumi na kuwapa wananchi fursa za kiuchumi.
āWananchi wa mikoa ya Kusini, ninawaletea salamu hizi za Rais wenu Samia Suluhu Hassan. Hizi barabara zikikamilika kutakuwa na taa za barabarani takribani 4800 kutoka Mtwara hadi Masasi. Kusini kutangāara kwa mwanga nyakati za usiku na kutapendeza. Kwenye barabara nzuri, uchumi unafunguka na kwenye mwanga kwa saa 24, biashara zinafanyika muda wote,āalisema Ulega.
Ulega yuko katika ziara ya kikazi mkoani Mtwara ambako pamoja na mambo mengine anafuatilia maagizo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya kuangalia maendeleo ya ukarabati wa barabara na miundombinu mingine ya ujenzi iliyoharibiwa wakati wa mvua za masika na kimbunga cha Hidaya kuanzia mwishoni mwa mwaka jana hadi mwaka huu.
Akitoa mchanganuo, Ulega alisema katika kiasi hicho cha fedha, zaidi ya shilingi bilioni 230 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Mnivata - Newala - Masasi (km 160) kwa kiwango cha lami pamoja na Daraja la Mwiti (m 84) ili kuzifungua Wilaya za Masasi, Newala, Tandahimba na Mtwara kiuchumi kupitia usafirishaji wa abiria na mazao.
āKazi kubwa inafanywa katika mikoa ya Kusini na ni dhamira ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuufungua Mkoa wa Mtwara ili mazao ya biashara na chakula yapate thamani kwa kufika katika masoko kwa urahisi pamoja na kupunguza gharama na muda wa usafiriā, amesisitiza Ulega.
Kuhusu faida nyingine za miradi hiyo ya ujenzi, Mbunge huyo wa Jimbo la Mkuranga aliwaambia wananchi wa mikoa ya Kusini kwamba wakandarasi waliopewa zabuni ya kujenga barabara hiyo watatakiwa pia kutia huduma nyingine kwa wananchi ikiwemo ujenzi wa ghala la kuhifadhia korosho, nyumba za madaktari na mambo mengine kwa mujibu wa mkataba.
Ulega amewataka wakandarasi wanaojenga barabara ya Mnivata-Masasi kuhakikisha wanatoa kipaumbele cha ajira kwa wananchi wazawa wa maeneo barabara inakopita kwa kushirikisha ofisi za Serikali za Mtaa na Kata za Wilaya.
Amesisitiza kuwa licha ya Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ya barabara, miradi hiyo inapaswa kuzalisha ajira kwa wananchi wazawa na kuacha ujuzi ili uweze kuwasaidia katika majukumu mengine ya kijamii na kiuchumi.
Ulega ameitaka TANROADS kukamilisha taratibu za kuwapata wakandarasi watakaotekeleza miradi Jumuishi ya kijamii (CSR) ili ujenzi wa barabara uende sambamba na miradi hiyo ambayo itahusisha ujenzi wa Kituo cha Mabasi, ghala, ununuzi wa mashine za kubangulia korosho, mabweni ya shule, ununuzi wa X-Ray na gari la wagonjwa.
Ulega ameeleza kuwa Rais Dkt. Samia ameshatoa kibali cha ukarabati wa barabara ya Mtwara hadi Mingoyo (Mnazi Mmoja) na Mingoyo hadi Masasi ambapo takribani Bilioni 152 zitatumika katika barabara hiyo.
Naye, Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Dotto John ameeleza mradi huo unaotekelezwa na Mkandarasi China WuYi umegawanywa katika sehemu mbili ambapo sehemu ya kwanza ya Mnivata - Mitesa (km 100) unatekelezwa kwa muda wa miezi 36 na sehemu ya pili ya Mitesa - Masasi (km 60) na ujenzi wa Daraja la Mwiti (m 84) unatekelezwa kwa muda wa miezi 30.
Kwa upande wake, Mbunge wa Tandahimba Ahmad Katani ameishukuru Serikali kwa mradi wa barabara hiyo kwani ni barabara ya kiuchumi kwa kuwa inapita katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa Korosho.