Rais Samia awaombea Mungu wanafunzi wa kidato cha sita walioanza mitihani yao ya mwisho leo
Eric Buyanza
May 6, 2024
Share :
Kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter) Rais Samia Suluhu Hassan ameandika haya;
“Nawatakia kila la kheri wanafunzi wote wa Kidato cha Sita mnaoanza mitihani yenu ya kuhitimu elimu ya sekondari leo. Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu awafanikishe katika hatua hii kwa mafanikio na kila jema katika hatua zinazofuata. Nina imani kuwa mmetumia muda wenu shuleni kujiandaa vyema, hasa baada ya Serikali kuamua kufuta ada kwa Kidato cha Kwanza hadi cha Sita, kujenga na kuboresha shule zaidi, ujenzi wa mabweni sehemu ambazo wanafunzi, hasa wa kike, walikuwa kwenye mazingira hatarishi na kuongeza Bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Uamuzi huu umeleta nafuu na faraja katika familia nyingi na ongezeko la watahiniwa zaidi kutoka 106,883 mwaka jana hadi 113,504 mnaoanza mitihani leo. Hatua mnayoanza leo ni muhimu katika safari yenu ya elimu na tunategemea vipawa, juhudi na kujituma kwenu kuleta mchango katika maendeleo ya nchi yetu kwa siku zijazo. Ahadi yangu ni kuendelea kufanya kazi, kupanga na kutekeleza mipango na sera ambazo zitawawezesha kutimiza nia yenu ya kuwa wananchi wenye mchango mkubwa kwa jamii na taifa letu ikiwemo; kuongeza fungu kwa wanafunzi zaidi kupata mikopo ya elimu ya juu na kuboresha sera na mazingira ya kukua kwa sekta binafsi ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa katika kuzalisha ajira nchini.”