Rais Samia Kugharamia matibabu ya Sativa.
Joyce Shedrack
July 2, 2024
Share :
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema atagharamia matibabu ya Kijana Edgar Mwakabela maarufu Sativa mpaka atakapona pamoja na kuhakikisha unafanyika uchunguzi wa tukio la utwekaji wa kijana huyo ambaye alitweka Jijini Dar es salaam June 23,2024 na kupatikana katika Hifadhi ya Katavi akiwa amejeruhiwa usiku wa kuamkia June 27,2024.
Hayo yamebainishwa kupitia tarifa iliyotolewa leo July 02,2024 na Kiongozi Mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe baada ya siku ya jana kumtembelea Kijana huyo aliyelazwa katika hospitali ya Aga Khan Jijini Dar es Salaam.
“Jana, July 01, 2024 nimepata nafasi ya kumtembelea Kijana aliyetekwa, kuteswa kwa kujeruhia vibaya kwa risasi Sativa, nimezungumza na Sativa, Ndugu zake pamoja na Watu wanaomhudumia, tangu Katavi mpaka sasa, nimeuona umoja wa kitanzania kwenye jambo hili, nawashukuru wote waliomchangia na wanaondelea kuchanga, hivi ndivyo inavyopaswa kuwa, aliyoyapitia yanaumiza na kusikitisha sana, yaliyomtokea Sativa ni lazima tuyakomeshe”
“Baada ya kutoka Hospitali, nilifanya jitihada za kumtafuta Rais wa Tanzania, kuzungumza nae, kumuelezea tukio la Sativa kutekwa, kupigwa risasi, na kutupwa msituni Katavi, pamoja na matukio mengine ya Watu kupotea, ambayo yamekithiri katika siku za karibuni, nimemueleza, yeye kama Rais na Amiri Jeshi Mkuu anao wajibu wa kulinda usalama wa Raia, na kwamba matukio ya namna hii yanachafua taswira na haiba yake, na yanaondoa murua wa R Nne zake (4R's)”
“Nimemsihi Ndugu Rais juu ya umuhimu wa yeye binafsi kuagiza ufanyike uchunguzi wa vyombo vya ulinzi na usalama ju ya tukio hili pamoja na mengine ya namna hii, kama Taifa tunahitaji kushirikiana pamoja kukomesha mambo ya Watu kutekwa, kuuawa, kupigwa na kutupwa misituni, yeye Rais anapaswa kuwa wa kwanza kwenye hili, Ndugu Rais amenisikiliza, na ameahidi kufanyia kazi ushauri wangu kwake”
“Kama hatua ya awali amenieleza kuwa yeye binafsi atabeba gharama zote za matibabu ya Sativa, kuanzia sasa mpaka atakapopona kabisa, pamoja na kuhakikisha unafanyika uchunguzi wa jambo hili, ninamshukuru Ndugu Rais kwa mwanzo huu, kila safari ndefu, inaanza na hatua ya kwanza, naamini sasa tutaanza safari ya kwenda kule tunakotaka, ambako tabia za kutekana zitakomeshwa” Imesema Taarifa hiyo aliyoitoa Zitto Kabwe.