Rais Samia kuzindua kituo cha Biashara Ubungo
Sisti Herman
July 17, 2025
Share :
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua Kituo Kikuu cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki (East Africa Commercial & Logistics Center - EACLC) mwezi Agosti 2, mwaka huu ikiwa ni miezi miwili kabla ya tarehe iliyokuwa imetarajiwa ya Oktoba, 2025.
Kituo hicho kikubwa kilichojengwa eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam, kimegharimu takriban dola za Marekani milioni 110 na kimetekelezwa kwa ushirikiano wa wawekezaji kutoka China. Lengo kuu la mradi huu ni kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na usambazaji bidhaa kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, huku kikichangia kukuza uchumi wa taifa na kukuza uwezo wa wafanyabiashara wa ndani.
Mradi wa EACLC utajumuisha maduka zaidi ya 2,060, ambapo asilimia 95 ya maduka hayo yamehifadhiwa kwa ajili ya wafanyabiashara wa Kitanzania, kuimarisha uwepo wa biashara za mitaani na zile za kisasa kwa kutumia teknolojia za kisasa za usimamizi na usafirishaji.
Mkurugenzi wa Kituo cha Biashara na Usafirishaji cha Afrika Mashariki, Cathy Wang, amesisitiza kuwa mradi huo umejengwa kwa malengo ya kukuza uchumi wa wananchi wa Tanzania na kuongeza ushindani wa wafanyabiashara wa ndani katika soko la kikanda.