Rais TAHLISO Atinga DIT kutatua changamoto ya wanafunzi kufanya mitihani
Sisti Herman
July 2, 2025
Share :
Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), Mheshimiwa Geofrey Kiliba amefanya ziara ya kikazi katika Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kufuatia taarifa kuhusu changamoto iliyokuwa ikiwakabili baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho waliohujika na ucheleweshwaji wa malipo ya ada.
Taarifa hizo zilieleza kuwa menejimenti ya chuo ilikuwa imetoa maelekezo kuwa wanafunzi wote waliochelewa kulipa ada ya masomo hawataruhusiwa kuingia katika mfumo ili kupata namba ya malipo, jambo ambalo lingewazuia kusajiliwa rasmi na hivyo kuwanyima fursa ya kushiriki katika mitihani ya mwisho wa muhula (Final Exams - FE).
Katika ziara hiyo, iliyofanyika Leo Tarehe 1 Julai 2025, Rais wa TAHLISO alikutana na viongozi wa Serikali ya Wanafunzi wa DIT wakiongozwa na Rais wao, Bwana Mlade ambapo walifanya kikao mahsusi kujadili hali halisi ya changamoto hiyo. Viongozi hao waliwasilisha kwa kina namna agizo hilo lilivyokuwa na athari kubwa kwa wanafunzi ambao kutokana na sababu mbalimbali za kiuchumi walishindwa kumaliza ada zao kwa wakati.
Baada ya kusikiliza hoja na maelezo ya kina kutoka kwa viongozi hao wa wanafunzi, Rais wa TAHILISO aliwasiliana moja kwa moja na uongozi wa chuo hicho kwa nia ya kutafuta suluhu ya haraka na ya kiutu. Katika mawasiliano hayo, Rais Kiliba aliomba chuo kutoa nafasi ya nyongeza ya muda kwa wanafunzi husika ili waweze kumalizia ada zao na hivyo kuruhusiwa kushiriki katika mitihani yao.
Kwa mshikamano, busara na maelewano, uongozi wa DIT ulikubali maombi hayo na kutoa nafasi ya mwisho ya siku mbili kwa wanafunzi wote waliokumbwa na changamoto hiyo, hatua ambayo imepokelewa kwa shukrani kubwa na wanafunzi husika.
TAHLISO inapenda kupongeza uongozi wa DIT kwa kusikiliza kilio cha wanafunzi na kuchukua hatua za kibinadamu zinazozingatia maslahi mapana ya elimu kwa vijana wa kitanzania. Pia tunawapongeza viongozi wa serikali ya wanafunzi wa DIT kwa ushirikiano wao katika kuhakikisha changamoto za wanafunzi zinatatuliwa kwa njia ya mazungumzo.
Rais wa TAHLISO anatoa wito kwa taasisi nyingine za elimu nchini kuiga mfano huu wa majadiliano na maelewano pale panapojitokeza changamoto zinazowahusu wanafunzi