Rais wa Iran awasili Marekani kwenye UNGA-81
Sisti Herman
September 23, 2026
Share :

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, amewasili nchini Marekani kushiriki Mkutano Mkuu wa 81 wa Umoja wa Mataifa (UNGA81).
Kuwasili kwa kiongozi huyo nchini Marekani ambayo kwa muda mrefu imekuwa katika mvutano mkubwa wa kisiasa na Iran, kunatokea katika kipindi ambacho viongozi wa Iran wameendelea kusisitiza umuhimu wa kushiriki katika majukwaa ya kimataifa, licha ya mazingira magumu ya kisiasa na kiusalama yanayoizunguka nchi hiyo.
Uamuzi wa viongozi wa Iran kushiriki katika mkutano huo umevuta hisia za wachambuzi na watu mbalimbali, hususan kwenye mitandao ya kijamii. Baadhi wameutafsiri uamuzi huo kama ishara ya kujiamini na msimamo wa Iran katika kuendelea kutumia diplomasia kama nyenzo ya kuwasilisha misimamo yake mbele ya jumuiya ya kimataifa.
Jumatatu, Septemba 21, 2026, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alitangulia nchini Marekani akiongoza ujumbe wa kidiplomasia wa taifa hilo.
Mkutano huo unatarajiwa kuwa jukwaa muhimu kwa Rais Pezeshkian kuwasilisha msimamo wa Iran kuhusu masuala mbalimbali ya kimataifa mbele ya viongozi wa dunia.
Macho ya jumuiya ya kimataifa sasa yanaelekezwa kwa ujumbe wa Iran, huku hotuba na hatua za Rais Pezeshkian zikitarajiwa kutoa picha ya mwelekeo wa diplomasia ya Tehran katika kipindi hiki cha mvutano wa kisiasa na Marekani.





