Rais wa Shirikisho la soka Congo atoroka Nchi kisa ufisadi.
Joyce Shedrack
March 31, 2026
Share :
Rais wa Shirikisho la Soka la Congo Brazzaville FECOFOOT Jean-Guy Blaise Mayolas, anaripotiwa kutoroka Nchi pamoja na familia yake baada ya kutiwa hatiani kwa ubadhirifu wa dola milioni 1.1 sawa na Bilioni 2.85 za FIFA.

Mayolas yuko mafichoni pamoja na mkewe na mwanawe baada ya wote kuhukumiwa kifungo cha maisha mwezi huu kwa ubadhirifu wa fedha zilizotolewa na shirikisho la soka duniani kama msaada wa kipindi cha Covid-19 mwezi Februari 2021.
Wachunguzi wanashuku huenda anajificha nchini Cameroon au Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mamlaka na vikosi vya polisi washirika katika eneo hilo vimearifiwa, na maafisa wanafanya kazi na vitengo vya ujasusi wa kifedha, ikiwemo Tracfin ya Ufaransa, ili kufungia mali zinazohusishwa na kesi hiyo.
Mayolas na wanafamilia wake walitiwa hatiani kwa utakatishaji fedha, kughushi, matumizi ya nyaraka bandia na ubadhirifu tarehe 10 Machi na mahakama ya Brazzaville, pamoja na katibu mkuu wa Fecofoot, Badji Mombo Wantete, na mweka hazina, Raoul Kanda. Wantete na Kanda walihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kila mmoja.
FIFA ilifungua taratibu za kinidhamu dhidi ya Mayolas, Wantete na Kanda wiki iliyopita kwa madai ya utovu wa nidhamu wa kifedha. Mashtaka yanayozingatiwa yanajumuisha mgongano wa maslahi, kughushi na kupokea zawadi isivyofaa baada ya kamati ya maadili ya Fifa kupokea taarifa na nyaraka wakati wa uchunguzi.





