Rais wa zamani wa Syria ahukumiwa kifo
Sisti Herman
August 12, 2026
Share :

Mahakama nchini Syria imemhukumu aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Bashar al-Assad, adhabu ya kifo baada ya kupatikana na hatia ya makosa mbalimbali yaliyohusishwa na ukandamizaji na vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyotikisa nchi hiyo kwa takribani miaka 14.
Hukumu hiyo ilitolewa Jumanne, Agosti 11, 2026, na inakuwa hukumu ya kwanza kubwa ya ndani dhidi ya Assad tangu kuondolewa kwake madarakani mwaka 2024.
Assad akuwapo mahakamani wakati wa kutolewa kwa hukumu hiyo. Tangu serikali yake kuangushwa mwezi Desemba 2024, amekuwa akiishi nchini Urusi baada ya kukimbilia huko kufuatia kuanguka kwa utawala wake.
Mahakama pia imemhukumu kifo Maher al-Assad, ambaye ni kaka yake Bashar, pamoja na Atef Najib, aliyekuwa mkuu wa usalama wa kisiasa katika mkoa wa Daraa na binamu wa Bashar al-Assad.
Tofauti na Bashar na Maher, Atef Najib alikuwepo mahakamani wakati hukumu ikisomwa. Najib alihusishwa na operesheni za ukandamizaji dhidi ya waandamanaji katika Daraa mwaka 2011, eneo ambalo lilikuwa miongoni mwa vituo vya mwanzo vya maandamano yaliyokuja kuchochea vita vya Syria.
Kwa mujibu wa taarifa za mahakama, mashtaka dhidi ya Assad yalihusisha mauaji, mateso, kukamatwa kiholela na uhalifu dhidi ya binadamu uliofanywa wakati wa vita vya Syria.





