Ramani mpya ya dunia na ukubwa halisi wa bara la Afrika
Sisti Herman
September 6, 2026
Share :

Ijumaa ya Septemba 4, 2026, imekuwa ni siku nyingine ya kukumbukwa katika historia ya Afrika baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) kuidhinisha matumizi ya ramani mpya ya dunia inayolenga kuonesha Bara la Afrika na maeneo mengine kwa uwiano wa ukubwa unaokaribiana zaidi na uhalisia.
Azimio hilo lililowasilishwa na Togo na kuungwa mkono na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), limepata kura 164 za ndiyo, huku Marekani ikiwa nchi pekee iliyopinga. Nchi sita hazikupiga kura.
Hatua hiyo inalenga kuhamasisha matumizi ya ramani zinazowakilisha kwa usahihi zaidi ukubwa wa mabara, baada ya mfumo wa ramani ya Mercator kutumika kwa karne nyingi katika kuonesha sura ya dunia.
Katika ramani mpya inayopendekezwa, Afrika inaonekana kwa ukubwa unaokaribiana zaidi na eneo lake halisi, tofauti na inavyoonekana katika ramani ya Mercator ambayo imekuwa ikikosolewa kwa kupotosha uwiano wa ukubwa wa maeneo mbalimbali duniani.
Ramani ya Mercator ilitengenezwa na mchora ramani wa Flemish, Gerardus Mercator, mwaka 1569. Ingawa mfumo huo ulisaidia sana katika urambazaji wa baharini, unaongeza ukubwa wa maeneo kadiri yanavyokaribia Ncha ya Kaskazini na Ncha ya Kusini.





