RC Mtanda atoa wito wa uboreshaji wa uwanja wa michezo Bariadi
Sisti Herman
November 24, 2026
Share :
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Said Mtanda, amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi kutenga bajeti kwa ajili ya maboresho ya uwanja wa michezo wa halmashauri hiyo, hatua inayolenga kuimarisha na kukuza shughuli za michezo mkoani humo.
Mtanda ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi kwenye uzinduzi wa Ligi ya Mkoa wa Simiyu uliofanyika katika uwanja huo, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuwa na miundombinu bora ya michezo inayoweza kuwasaidia wanamichezo kufanya vizuri.
Amesema maboresho ya uwanja huo ni muhimu katika kuweka mazingira rafiki kwa wanamichezo, mashabiki pamoja na wadau mbalimbali wa michezo, huku yakichangia kuongeza hamasa na ushiriki wa wananchi katika shughuli za michezo.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amesisitiza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya michezo ni sehemu ya juhudi za kukuza vipaji vya vijana, kuwawezesha kushiriki katika mashindano mbalimbali na kutumia michezo kama njia ya kujenga afya, nidhamu na mshikamano katika jamii.
Uzinduzi wa Ligi ya Mkoa ni hatua muhimu katika kuendeleza michezo mkoani Simiyu, huku agizo la kutenga bajeti ya maboresho ya uwanja likitarajiwa kuwa chachu ya kuboresha mazingira ya michezo na kuongeza ushindani kwa timu zinazoshiriki ligi hiyo.





