Real Madrid yamnyatia Scott Mctominay wa Napoli
Eric Buyanza
October 9, 2026
Share :

Miamba ya soka ya Uhispania, Real Madrid, imeingia rasmi kwenye mbio za kuwania saini ya kiungo wa kimataifa wa Scotland na SSC Napoli, Scott McTominay (29), kufuatia kuripotiwa kukwama kwa mazungumzo ya mkataba wake mpya nchini Italia.
Taarifa kutoka vyombo vya habari vya Italia kama Tuttomercatoweb na gazeti la The Sun la Uingereza zinasema kuwa Real Madrid tayari imewasiliana na wawakilishi wa mchezaji huyo ili kufuatilia kwa karibu mwenendo wake.
Kiungo huyo, ambaye amekuwa tegemeo muhimu tangu ajiunge na SSC Napoli akitokea Manchester United, anaripotiwa kutaka mshahara wa karibu Euro milioni 8 (takriban Shilingi za Tanzania Bilioni 23.64) kwa mwaka, hata hivyo kiwango hicho kinazidi kiwango cha juu cha mshahara kilichowekwa na uongozi wa Napoli chini ya Rais Aurelio De Laurentiis, hali inayofanya klabu hiyo kusita kuafiki masharti hayo mapya kwa mchezaji anayeelekea umri wa miaka 30.
Nia ya Real Madrid kuongeza nguvu kwenye safu yao ya kiungo inachangiwa zaidi na uwepo wa kocha José Mourinho kwenye benchi la ufundi la miamba hiyo ya La Liga. Mourinho ndiye aliyemgundua na kumpandisha McTominay katika kikosi cha kwanza wakati wakiwa pamoja Manchester United na anafahamika kuvutiwa sana na uwezo wake wa kimbinu pamoja na nidhamu ya mchezo.





