Red Eyes yasambaa mikoa 17, waathirika zaidi ya elfu 5
Sisti Herman
January 29, 2024
Share :
Serikali kupitia Wizara ya Afya, imesema jumla ya mikoa 17 nchini imekumbwa na ugonjwa wa macho mekundu ujulikanao kitaalamu kama viral keratoconjunctivitis (red eyes) na watu 5,359 wametajwa kuathirika.
Kufuatia kusambaa huko, wizara imewaasa wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo unaosababishwa na maambukizi ya kirusi kwenye ngozi ya juu ya gololi ya jicho.
Takwimu hizo zimetajwa leo Jumatatu, Januari 29, 2024 na Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya, Profesa Paschal Rugajjo alipokuwa akitoa taarifa kuhusu hali ya ugonjwa huo kwa sasa.
Amesema hadi kufikia Ijumaa Januari 26, idadi ya waliofika kwenye vituo vya afya walifikia 5,359 kutoka wagonjwa 1,109 Januari 19.
“Ugonjwa huu umesambaa zaidi ingawaje ni wachache ndiyo wanafika vituo vya huduma za afya, mpaka sasa ugonjwa huu umesambaa na kuongezeka katika mikoa 17 ikiwemo ya Singida, Katavi, Kilimanjaro, Mara, Iringa, Njombe, Ruvuma, Simiyu, Mtwara, Lindi, Songwe, Rukwa na Mwanza,” amesema alipozungumza na Mwananchi.
Amesema awali ugonjwa huo ulikuwepo katika mikoa minne ikiwemo Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma na Pwani.