Refa atolewa nje, atuhumiwa kuchezesha akiwa amelewa
Eric Buyanza
November 26, 2026
Share :

Tukio la kustaajabisha limetokea katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Asia Daraja la Pili (AFC Champions League Two) jana Jumatano, Novemba 25, 2026, baada ya mwamuzi wa kati raia wa Syria, Hanna Hattab, kuondolewa uwanjani wakati wa mapumziko kutokana na tuhuma za kuchezesha mechi akiwa amelewa.
Tukio hilo lilitokea katika mchezo uliomalizika kwa klabu ya Al Jazira ya Falme za Kiarabu kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Gol Gohar ya Iran.
Utata ulianza katika dakika ya 32 ya kipindi cha kwanza baada ya mchezaji wa Gol Gohar, Ali Asghar Ashouri, kuchezewa madhambi katikati ya uwanja. Badala ya kumuadhibu mchezaji aliyefanya kosa hilo, mwamuzi Hattab alipigwa na butwaa kwa muda kisha akamwita golikipa wa Al Jazira, Ersin Destanoğlu—ambaye hakuwa karibu na tukio hilo—na kumuonyesha kadi ya njano.
Uamuzi huo uliwaacha vinywa wazi wachezaji na mashabiki uwanjani, hali iliyosababisha mchezo kusimama kwa takriban dakika nne. Baada ya kushauriana na mwamuzi wa akiba (fourth official), Hattab alibatilisha uamuzi wake na kuifuta kadi hiyo.
Hali ya mambo ilizidi kuwa tete kuelekea mapumziko, ambapo kocha mkuu wa Gol Gohar, Mehdi Rahmati, alinaswa na kamera akipiga kelele kuwa mwamuzi huyo "amelewa". Klabu hiyo ya Iran ilitishia kutorudi uwanjani kuendelea na kipindi cha pili endapo mwamuzi huyo asingeondolewa, ikidai hakuwa katika hali yake ya kawaida.





