Ronaldinho arejea uwanjani akiwa na miaka 46 asaka bao lake la 300
Eric Buyanza
August 21, 2026
Share :

Gwiji wa soka wa Brazil, Ronaldinho Gaúcho, amerejea rasmi kwenye soka la ushindani akiwa na umri wa miaka 46 baada ya kusaini mkataba na klabu ya Ravenna FC inayoshiriki Serie C (daraja la tatu) nchini Italia.
Klabu hiyo inamilikiwa na rafiki yake, mfanyabiashara Ignazio Cipriani.
Hii ni miaka 11 tangu acheze mechi yake ya mwisho ya kulipwa mnamo mwaka 2015 akiwa na timu ya Fluminense ya Brazil.
Mbali na kusajiliwa kama mchezaji, atakuwa pia mwanahisa mdogo na balozi wa kuitangaza klabu hiyo kibiashara.
Rais wa klabu hiyo amethibitisha kuwa Ronaldinho atacheza angalau mechi moja rasmi au chache tu, hatakuwa mchezaji wa kutumika kila wiki kwasababu kurejea kwake uwanjani una malengo maalum ya kibiashara.
Ronaldinho mwenyewe amesema dhamira yake kubwa ni kutaka kufunga bao lake la 300 katika maisha yake ya soka, itakumbukwa Gwiji huyu alistaafu soka la ushindani akiwa amefunga jumla ya mabao 299 katika mechi rasmi za ngazi ya klabu na timu ya taifa ya Brazil.





