Ruben Neves bado anazungumza na rafiki yake Diogo Jota.
Joyce Shedrack
June 27, 2026
Share :
Ruben Neves amefichua kuwa bado anaendelea kumtumia ujumbe Diogo Jota, karibu mwaka mmoja baada ya nyota huyo wa Liverpool kufariki dunia kwa ajali ya gari.
Jota alifariki akiwa na umri wa miaka 28 pamoja na kaka yake Andre Silva mnamo Julai 3, 2025, baada ya gari lake aina ya Lamborghini kupata ajali katika jimbo la Zamora nchini Hispania.

Aliyewahi kuwa mchezaji mwenzake na rafiki yake wa karibu katika klabu za Porto na Wolves kati ya mwaka 2016 na 2020, pamoja na timu ya taifa ya Ureno amezungumzia jinsi anavyokabiliana na majonzi ya kumpoteza rafiki yake.
"Bado nazungumza naye. Watu wachache sana wanajua hili.Tuna kundi la WhatsApp ambalo lipo pamoja na Rute (mjane wa Jota) na Diogo, na bado lipo, na tunaendelea kuwasiliana humo. Kila jambo maalum linapotokea, huwa ninatumia ujumbe kwenye WhatsApp yangu".
Neves pia alieleza kuwa siku iliyofuata baada ya kupata habari za kifo cha Jota ilikuwa "siku ngumu zaidi" katika maisha yake.
Kauli hizi zimekuja baada ya mjane wa Jota, Rute Cardoso, kuadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja wa ndoa yao wiki iliyopita kwa kushiriki hotuba ambayo Jota alitoa siku ya harusi yao.





