Sadio Mane atangaza kustaafu kucheza Timu ya Taifa.
Joyce Shedrack
July 10, 2026
Share :
Nahodha na nyota wa Senegal, Sadio Mané ametangaza rasmi kustaafu soka la kimataifa, akihitimisha safari yake ya kuitumikia timu ya taifa baada ya miaka mingi ya mafanikio makubwa.

Mané anaondoka akiwa mmoja wa wachezaji bora zaidi kuwahi kuichezea Senegal akiwa amefunga mabao 54 na kutoa pasi za mabao 29 katika kipindi chote cha kuitumikia timu hiyo.
Katika mafanikio yake makubwa akiwa na Senegal, Mané aliiongoza nchi yake kutwaa taji la Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2022 huku pia akimaliza nafasi ya pili mara mbili kwenye mashindano hayo.
Kwa upande wa tuzo binafsi, mshambuliaji huyo alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa AFCON mara mbili na kutangazwa kuwa Mwanasoka Bora wa Afrika mara mbili, jambo linalothibitisha nafasi yake kama mmoja wa wachezaji wakubwa zaidi katika historia ya soka la Afrika.
Kustaafu kwa Mané kunafunga ukurasa wa mafanikio makubwa kwa Senegal, huku akiacha urithi mkubwa ambao utaendelea kukumbukwa na vizazi vya sasa na vijavyo vya wapenzi wa soka.





