Safari ya ndege yasitishwa baada ya mtoto kugoma kukaa
Eric Buyanza
August 10, 2026
Share :
Ndege ya shirika la ndege la Porter Airlines huko Amerika Kaskazini ililazimika kurudishwa kwenye maegesho yake na baadae kufuta safari baada ya mtoto mdogo kusimama kwenye kiti chake na kukataa kukaa wala kufunga mkanda wakati ndege hiyo ikijiandaa kuondoka.
Ilikuwa hiviiii...
Ndege ilikuwa tayari imeshaondoka kwenye lango la kupandia na kuanza kusogea kuelekea njia ya kurukia (runway).
Mhudumu wa ndani ya ndege akabaini kuna mtoto mdogo amesimama juu ya kiti huku akikataa katakata kuketi na kufunga mkanda licha ya juhudi zilizofanywa na wazazi wakishirikiana na mhudumu huyo.
Kutokana na ukaidi huo unaohatarisha usalama, marubani waliamua kugeuza ndege na kwenda kushusha abiria wote, jambo lililosababisha usumbufu mkubwa.
Kulingana na sheria za usafiri wa anga za kimataifa, hakuna ndege inayoruhusiwa kupaa au kutua ikiwa kuna abiria (hata awe mtoto) ambaye hajafunga mkanda wa usalama.






