Sakata la Mrisho Gambo kupelekwa kamati ya maadili ya Bunge.
Joyce Shedrack
April 23, 2025
Share :
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, ameagiza suala la mvutano kati ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa na Mbunge wa Arusha Mjini Mhe. Mrisho Gambo, kupelekwa mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili kuchunguzwa.
Hii nikufuatia madai yaliyoibuliwa na Mbunge wa Arusha Mjini Mrisho Gambo Jumatano ya wiki iliyopita wakati wa mjadala wa bajeti ya TAMISEMI Bungeni jijini Dodoma alipoeleza kuwepo kwa matumizi mabaya ya fedha za Umma katika ujenzi wa jengo la utawala mkoani Arusha.
Spika wa Bunge Dkt.Tulia alitoa maelekezo kwa Waziri Mchengerwa kufuatilia tuhuma hizo na kutoa majibu kwa Bunge.
Siku ya jana Waziri Mhe. Mchengerwa wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya wizara yake alisema hakuna pesa za Watanzania zilizopotea katika miradi yote miwili ndani ya Jiji la Arusha.
Hata hivyo Mbunge wa Arusha Mrisho Gambo hakuridhishwa na majibu hayo yaliyotolewa na Waziri wa TAMISEMI na kusema taarifa hizo hazikuwa za kweli na zilidanganya Bunge.
Leo Mhe. Mchengerwa, aliwasilisha tena maelezo ya ziada kufuatia agizo la Spika lakini Mbunge huyo alisimama tena na kusisitiza kwamba baadhi ya maeneo ya taarifa hiyo bado hayana ukweli.
Kutokana na mvutano huo Spika wa Bunge Mhe. Dkt. Tulia Ackson, ameamuru suala hilo lipelekwe rasmi kwenye Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kwa uchunguzi wa kina na taarifa kamili itolewe ndani ya wiki moja kuanzia leo.