Scaloni afungua milango kwa Messi kuwa kocha msaidizi Argentina
Eric Buyanza
November 17, 2026
Share :

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Argentina, Lionel Scaloni, amesema milango iko wazi kwa nahodha wa zamani wa kikosi hicho, Lionel Messi, kujiunga na benchi lake la ufundi wakati wowote atakaotaka.
Scaloni alitoa kauli hiyo katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Costa Rica, huku akimtania nyota huyo mwenye umri wa miaka 39 kufuatia kuondoka kwa aliyekuwa kocha msaidizi, Walter Samuel, ambaye ameamua kwenda kuanza safari yake mpya kama kocha mkuu.
"Nadhani ataendelea kucheza soka hata baada ya mwaka 2030. Tayari ameshasema hatacheza tena timu ya taifa, lakini kama mchezaji, natumai ataendelea kucheza kwa muda mrefu kadiri awezavyo," alisema Scaloni. "Lakini kwa kuwa Walter hayupo tena, akitaka kuja hapa hakuna tatizo lolote, anakaribishwa wakati wowote," aliongeza kocha huyo kwa utani na kicheko.
Ingawa kauli hiyo ilitolewa katika hali ya ucheshi, imeonesha heshima na uhusiano wa karibu uliopo baina ya Scaloni na Messi.





