Serikali kusafirisha Mashabiki wa Yanga kwenda Sauzi bure
Sisti Herman
April 1, 2024
Share :
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo imekubali ombi la Uongozi wa klabu ya Yanga la kusafirisha mashabiki kwaajili mchezo wa marudiano kati ya Yanga dhidi ya Mamelodi Sundowns utakaocheza Ijumaa hii nchini Afrika kusini.
Rais wa Klabu ya Yanga Eng. Hersi Said wakati akitoa taarifa hiyo alisema;
"Tunafahamu Klabu yetu ya Young Africans SC ina mchezo mwingine wa pili kule Afrika Kusini hivyo Uongozi wenu umefanya jitihada za kupeleka Ombi katika Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo chini ya Waziri wetu Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro la kusafirisha mashabiki kwa njia ya Basi na tunaishukuru Wizara kwa kukubali Ombi letu".
"Wizara itahudumia gharama zote za safari ya kuelekea Afrika kusini yenye Wanachama na Mashabiki wetu 48 kuanzia Nauli mpaka pesa ya kujikimu, hivyo sisi Young Africans tunaishukuru sana Wizara".
"Hapo mwanzo tulitangaza watu watakaosafiri walipaswa kuwa na shilingi laki 6 na tulipata watu 30, niwahakikishie baada ya Wizara kukubali kusafirisha Wanachama na Mashabiki wetu,zile laki 6 zitarudishwa kwa wenyewe".
Kwa upande wa Wizara Naibu Waziri wa Wizara ya Utamaduni, sanaa na michezo Hamis Mwinjuma "Mwana FA" aliongeza;
"Kwanza niwapongeze sana kwa uamuzi wa kusafiri kwa basi kwani mngeweza kusema mbaki nyumbani na kutazama mechi kwenye Tv, Hii inamaanisha nyinyi ni wafia Yanga, Hongereni sana.
Uzuri kiwango cha timu yetu mmekiona na kinaridhisha, mpinzani tunayekwenda kucheza naye hana faida ya Mashabiki wengi hivyo naamini Nguvu ya kushangilia ambayo mnayo itakwenda kuleta tija kwenye mchezo wetu siku ya ijumaa.
Nimekuja hapa kufikisha salamu za Serikali chini ya Daktari Samia Suluhu Hassan, kila kinachoendelea yeye anafuatilia kwa umakini na anawatakia kila la heri kwenye Safari hii na kwenye mchezo wetu siku ya ijumaa" Naibu Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Hamis Mwinjuma