Serikali kuwainua wachimbaji wadogo
Sisti Herman
June 14, 2026
Share :

Serikali imesisitiza kufanyia kazi kwa haraka Mapendekezo yaliyotolewa na Timu ya Wataalamu iliyoundwa Kuishauri Wizara ya Madini kuhusu namna ya Kuwaendeleza Wachimbaji Wadogo Kiuchumi na kueleza kuwa, utatuzi wa changamoto za Mitaji, Teknolojia na upatikanaji wa taarifa sahihi za Kijiolojia kwa Wachimbaji Wadogo wa Madini ni hatua muhimu ya kuongeza ajira kwa watanzania, kupunguza umaskini na kukuza uchumi wa Taifa kuelekea Dira 2050.
Hayo yamebainishwa Juni 13, 2026 jijini Dar Es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, wakati wa hafla ya Kupokea Mapendekezo ya Kuwaendeleza Wachimbaji Wadogo Nchini na kusisitiza kwamba, maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha mipango ya maendeleo inajibu changamoto tatu kuu za taifa ambazo ni kuongeza mitaji kwa wananchi, kuzalisha ajira na kupunguza umaskini.
Amesema kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata mitaji na teknolojia, kunafungua fursa za kuongeza uzalishaji, ajira na kipato cha wananchi na kuongeza kuwa hiyo ndiyo njia mojawapo ya kupambana na umaskini.
‘’Kazi kubwa ya Waziri ni kutoa mwelekeo wa kisera wa taasisi au wizara anayoiongoza. Kwa muda niliokaa kwenye Wizara yangu, Mhe. Mavunde amekua akijua kipaumbele anachokitaka na jinsi ya kukipata,’’amesisitiza Prof. Mkumbo.
Ameongeza kwamba, hali ya umaskini nchini bado ipo kwa kiwango cha juu na kutolea mfano wa Mkoa wa Geita ambao unaoongoza kwa shughuli za uchimbaji madini ya dhahabu nchini ambapo hali ya umaskini inafikia asilimia 38 na kusisitiza kwamba, wachimbaji wadogo wanapowezeshwa wanasaida kutatua changamoto kama hizo na kuongeza kuwa, Sekta ya Madini imewekwa kama moja ya sekta muhimu za kimageuzi inayotarajiwa kuchangia kwenye ukuaji wa uchumi.





