SGR kuanza safari za Express Dar-Moro, haisimami vituo vya kati
Eric Buyanza
July 1, 2024
Share :
TAARIFA KWA UMMA: MABADILIKO YA RATIBA NA ONGEZEKO LA SAFARI ZA TRENI ZA SGR KUANZIA TAREHE 5 JULAI 2024
Shirika la Reli Tanzania - TRC linautaarifu umma kuhusu mabadiliko ya ratiba na ongezeko la safari za treni za reli ya kiwango cha kimataifa - SGR kati ya Dar es Salaam na Morogoro kuanzia tarehe 5 Julai 2024.
Ongezeko la Safari litahusisha kuanza kwa treni mpya ya haraka (Express train) ambayo itakuwa ikifanya safari kati ya Dar es Salaam na Morogoro bila kusimama vituo vya kati.
Mabadiliko ya ratiba yatakuwa kama ifuatavyo; Treni ya haraka itakuwa ikiondoka Dar es Salaam saa 12:00 asubuhi na saa 1:10 usiku. Treni itaondoka Morogoro saa 12:20 asubuhi na saa 1:30 usiku.
Treni ya kawaida itakuwa ikiondoka Dar es Salaam saa 3:30 asubuhi na saa 10:00 jioni na itaondoka Morogoro saa 3:50 asubuhi na saa 10:20 jioni.
Abiria anashauriwa kukata tiketi kupitia njia ya mtandao au madirisha ya tiketi yaliyo ndani ya vituo vya treni saa 2 kabla ya muda wa safari ili kuepuka msongamano.
Shirika litaendelea kuongeza idadi ya safari kulingana na ongezeko la idadi ya abiria ili kutoa huduma bora na za uhakika.
Jamila Mbarouk
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano