Sheikh Mansoor ashinikizwa kuiuza Man City
Eric Buyanza
May 12, 2026
Share :

Serikali ya Uingereza imetakiwa kuzingatia vikwazo dhidi ya mmiliki wa Manchester City Sheikh Mansour bin Zayed Al-Nahyan kutokana na mzozo wa kivita unaoendelea nchini Sudan.
Mansour ameibadilisha klabu ya Manchester tangu ainunue mwaka 2008, na kufikisha mataji manane ya Ligi Kuu ya Uingereza, taji moja la Ligi ya Mabingwa, mataji matatu ya FA na mataji saba ya Kombe la Ligi.
Ripoti zinasema shirika la haki za binadamu la FairSquare limetoa wito hivi karibuni kwa Ofisi ya Mambo ya nje ya Serikali ya Uingereza kuzingatia vikwazo na kuchunguza kazi za Sheikh Mansour bin Zayed Al-Nahyan, Mmiliki wa Manchester City na Naibu Waziri Mkuu wa Nchi ya Falme za Kiarab UAE, katika madai ya Serikali hiyo kuunga mkono kundi la wanamgambo linalotuhumiwa kufanya uhalifu wa kivita nchini Sudan.
Wakati hayo yakijili, Serikali ya UAE inakanusha vikali kuwa mhusika katika mzozo huo.
FairSquare wanadai iwapo serikali ya Uingereza itaamua kumuwekea vikwazo Mansour, ataondolewa kwenye umiliki wa Manchester City, chini ya sheria za Ligi Kuu ya Uingereza.





