Si kila uvimbe ni saratani na wengi hupona - Dk. Kaguo
Eric Buyanza
July 4, 2026
Share :

Hospitali ya Taifa Muhimbili inaendelea kutoa huduma za upasuaji kwa wagonjwa wenye uvimbe mbalimbali katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), kupitia chumba cha upasuaji kinachotembea (mobile theatre).
Akizungumza mara baada ya kumfanyia upasuaji mgonjwa wa tatu katika maonesho hayo, Daktari Bingwa wa Upasuaji kutoka Muhimbili, Dk. Jenikalo Kaguo, amesema hospitali hiyo imejipanga kutoa huduma za kibingwa katika mazingira ya kidigitali ili kuwafikia wananchi kwa haraka zaidi.
Amesema huduma zinazotolewa zinahusisha upasuaji wa uvimbe mbalimbali wa tumboni na maeneo mengine ya mwili, lengo likiwa ni kuhakikisha wagonjwa wanapata matibabu kwa wakati bila kuchelewa.
Dk. Kaguo amewatoa wasiwasi wananchi wenye hofu kwamba upasuaji wa uvimbe ni sawa na hukumu ya kifo, akifafanua kuwa si kila uvimbe ni saratani na wengi hupona kabisa baada ya matibabu sahihi.
Amesema wananchi wanapaswa kujitokeza katika maonesho hayo ili kupata huduma za kibingwa bila hitaji la rufaa, jambo linalorahisisha upatikanaji wa matibabu kwa haraka zaidi.
“Tunawakaribisha wagonjwa wote wenye changamoto za uvimbe wafike wapate huduma, hapa tunawafikia moja kwa moja bila kuchelewa,” amesema Dk. Kaguo.
NIPASHE





