“Sifanyi kila kitu ambacho Trump anataka” - Netanyahu
Eric Buyanza
June 22, 2026
Share :

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema kuwa watu wengi hudhani yeye na Rais wa Marekani, Donald Trump, hufanya kazi kwa ushirikiano wa karibu katika kila jambo, lakini si kweli kwamba kila mara wanaafikiana.
Netanyahu aliongeza kuwa si wakati wote hufuata matakwa ya Marekani, akisisitiza kuwa Israel hufanya maamuzi yake kwa kuzingatia maslahi yake ya kitaifa.
Kauli hiyo imekuja baada ya Trump pamoja na Makamu wa Rais wa Marekani, J. D. Vance, kumkosoa hadharani.
Akizungumza katika Mkutano wa Kimataifa wa Sera uliofanyika mjini Jerusalem, Netanyahu alisema hataruhusu Iran kupata silaha za nyuklia na kwamba majeshi ya Israel yataendelea kuwepo kusini mwa Lebanon kwa muda wowote utakaoonekana kuwa wa lazima kwa usalama wa nchi yake.
Akihutubia Mkutano wa JNS mjini Jerusalem, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alisema:
“Nchini Marekani, watu husema kwamba Rais Trump hufanya kila ninachomwambia afanye. Nchini Israel, watu hudhani kwamba mimi hufanya kila anachotaka Trump. Lakini hakuna kati ya mambo hayo yaliyo ya kweli.”
Netanyahu alitumia kauli hiyo kusisitiza kwamba yeye na Rais wa Marekani, Donald Trump, wanafanya maamuzi kwa kujitegemea kulingana na maslahi ya nchi zao, na si kwamba mmoja humwelekeza au kumdhibiti mwingine.
"Sisi ni viongozi wa mataifa huru na yenye fahari. Wakati mwingine maoni yetu hutofautiana. Kila mmoja wetu anasimamia maslahi ya nchi yake. Mimi ninasimamia maslahi na usalama wa Israel."
Netanyahu aliendelea kusema:
"Mara nyingi mawazo yetu yanaendana. Lakini wakati mwingine hayaendani. Tunaheshimu mamlaka ya kila mmoja, uongozi wa kila mmoja, na dhamira ya kila mmoja kwa wananchi wake."
Kauli hiyo ya Benjamin Netanyahu ilikuwa ikisisitiza kwamba licha ya uhusiano wa karibu kati ya Israel na Marekani, yeye na Rais wa Marekani, Donald Trump, hawakubaliani katika kila jambo na kila mmoja hufanya maamuzi kwa kuzingatia maslahi ya taifa lake.
BBC





