Siku Vincent Aboubakar alipoishangaza dunia mbele ya Brazil!
Eric Buyanza
November 9, 2026
Share :

Picha hii inaonesha moja ya matukio ya kuchekesha na ya kihistoria katika Kombe la Dunia la FIFA 2022, ambapo mshambuliaji wa Kameruni, Vincent Aboubakar, alipewa kadi nyekundu kwa kusherehekea goli kwa hisia kali lakini kwa namna ya kipekee kabisa!
Picha linaanza hivi, ilikuwa tarehe 2 Desemba 2022. Cameroon vs Brazil. Kwenye karatasi, kila mtu alijua Brazil "anaua mtu." Dakika zikaenda, 90 zikaisha zikiwa 0-0. Mashabiki wa Kameruni wameshika roho mkononi, Brazil wanashambulia kama nyuki.
Kisha, dakika ya 92 (dk za nyongeza) Jerome Ngom Mbekeli akapiga juu krosi moja safi sana. Vincent Aboubakar akapaa angani kama tai na kupiga kichwa kikali kilichomwacha kipa wa Brazil akidaka hewa! Goli! Kameruni 1, Brazil 0! Dunia nzima ikasimama!
Hapo ndipo akili ya Aboubakar ilipohama kwa muda, Kwa furaha iliyopitiliza, Aboubakar aliona jezi inamnyima uhuru. Akaivua na kukimbia uwanjani kifua wazi akishangilia ushindi wa kihistoria dhidi ya miungu wa soka, Brazil!
Kwenye soka, ukivua jezi ni kadi ya njano automatically. Tatizo ni kwamba Aboubakar alikuwa tayari ana kadi nyingine ya njano mfukoni. Hesabu rahisi: Njano + Njano = Nyekundu! ?
Mwamuzi wa mechi hiyo, Ismail Elfath, alijikuta kwenye wakati mgumu zaidi wa kazi yake. Alimwendea Aboubakar huku akicheka. Ni kama alikuwa anamwambia: "Mwanangu, umeupiga mwingi sana, goli la hatari... lakini sheria ni sheria, inabidi uende benchi."
Mwamuzi alimpa mkono wa pongezi, kisha akampa kadi nyekundu. Aboubakar, badala ya kukasirika au kulalamika kama wachezaji wengine wanavyofanya wakipewa kadi nyekundu, alicheka, akamshika mkono mwamuzi, na kuanza kuondoka uwanjani kwa madoido akitabasamu! Aliondoka kama mtu aliyemaliza vita na kushinda.
Aboubakar alikua mchezaji wa kwanza katika historia ya Kombe la Dunia kufunga goli na kupewa kadi nyekundu kwenye mechi hiyo hiyo tangu Zinedine Zidane afanye hivyo mwaka 2006.
Licha ya kwamba Kameruni walitolewa kwenye mashindano siku hiyo, Aboubakar aliondoka Qatar akiwa ametengeneza historia ambayo mashabiki wa soka hawatakuja kuisahau!





