Simba jike ambananisha mkulima kwa nusu saa bila kumdhuru
Eric Buyanza
July 8, 2026
Share :

Mkulima na mfugaji wa ng'ombe nchini India amenusurika kifo baada ya simba jike kumwangusha chini na kumkalia kwa takriban dakika 30 bila kumshambulia.
Tukio hilo, lililonaswa katika video, linaonyesha simba huyo ambaye bado ni kijana akiwa amekaa juu ya mfugaji huyo aliyefahamika kwa jina la Kalu Parmar, huku akiwa amelala kimya bila kufanya harakati zozote.
Wakati huo, wakazi wa eneo hilo walikusanyika wakipiga kelele na kurusha mawe kwa lengo la kumfukuza simba huyo na kumuokoa Parmar.
Hadi sasa, hakuna anayejua sababu iliyomfanya simba huyo kutomshambulia mfugaji huyo.
Kwa upande wake, Parmar amesema anaamini alinusurika kwa sababu alibaki mtulivu na alikuwa akimpapasa simba huyo taratibu, jambo ambalo huenda lilimfanya mnyama huyo kutomdhuru.
Tukio hilo limeibua mjadala kuhusu tabia za wanyamapori na namna ya kujikinga wakati wa kukutana na wanyama wakali porini.
Akisimulia mkasa huo, Kalu Parmar alisema:
"Nilikuwa naelekea kuwapa chakula ng'ombe wangu wakati simba jike aliponivamia ghafla kutoka nyuma. Aliudaka mkono wangu na kunikalia na hakuniachia kwa muda mrefu."
Baada ya kuokolewa, Parmar alipelekwa katika hospitali ya eneo hilo kwa ajili ya kupatiwa huduma ya kwanza kabla ya kuhamishiwa hospitali maalumu kwa matibabu zaidi.





