Simba na JKT kuamua Bingwa ligi ya wanawake leo
Sisti Herman
April 29, 2024
Share :
Baada ya kuwatawala watani zao Yanga Princess kwenye ligi ya Wanawake kwa kuwafunga mabao 3-1, Simba Queens leo itashuka Uwanja wa Azam Complex Chamazi kukipiga na JKT Queens leo saa 10:00 Jioni.
Hadi sasa Simba inaongoza msimamo wa ligi na pointi 34, ikifuatiwa na JKT na pointi 28 baada ya kupokwa pointi tano kama adhabu baada ya kutotokea uwanjani huku Yanga Princess ikisalia nafasi ya tatu na pointi 21.
Ni mchezo muhimu kwa timu zote mbili kuamua hatma ya ubingwa Simba ikijiweka kwenye nafasi nzuri vivyo hivyo kwa JKT ambayo inataka kutetea taji hilo.
Zilipokutana timu hizo msimu uliopita, JKT ilivuna pointi nne ikishinda mabao 2-1 ugenini na kutoa sare ya bao 1-1 nyumbani lakini msimu huu tayari imepoteza pointi tatu na ngao ya jamii ambayo Simba ilibeba kombe hilo kwa mikwaju ya penati 5-4 dakika 90 zikiisha kwa sare ya 1-1 Azam Complex Chamazi.
Licha ya Simba kutopoteza mchezo wowote lakini udhaifu upo kwa kipa wao, Carolyne Rufa ambae amekuwa mbovu kwenye mipira ya mbali ambayo kwenye mabao saba walioruhusu mabao matano ya mbali lakini kwa upande wa JKT wamekuwa bora huku kukiwa na madhaifu kwa mabeki wa pembeni, Happyness Mwaipaja na Fatuma Makusanya.
Hii ni nafasi kwa mastraika wote wawili wa timu hizo kuonyesha umahiri wao, Stumai Abdallah (JKT Queens) ambaye ndio kinara wa wafungaji akiwanayo 17 huku Aisha Mnunka (Simba Queens) akifunga 15.