Simba yamshusha Mzimbabwe
Sisti Herman
January 5, 2024
Share :
Inasemekana klabu ya Simba imemaliza usajili wa ndani na sasa imehamia anga ya kimataifa baada ya usiku wa kuamkia jana kushusha mashine kimyakimya tayari kwa kuboresha kikosi hicho kilichopo kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa sasa visiwani Zanzibar.
Simba imemshusha fundi Michael Charamba (27) raia wa Zimbabwe, anayemudu nafasi tofauti kwa eneo la mbele ambaye inaelezwa ni pendekezo la Kocha Abdelhak Benchikha. Huyo ni staa wa kwanza wa kigeni kwa Simba kwenye dirisha dogo kushushwa baada ya awali kutambulishwa Saleh Masoud Karabaka kutoka JKU, huku ikielezwa pia imemalizana na Ladeck Chasambi kutoka Mtibwa Sugar na Edwin Balua kutoka TZ Prisons ikiwa ni wachezaji wa ndani.
Charamba aliyeitumikia Chicken Inn ya Zimbabwe anasifika kama kiraka ambaye amekipa kikosi hicho ubora mkubwa kutokana na kumudu kucheza nafasi ya straika, kiungo mshambuliaji, na winga wa kulia.
Zaidi ya hayo jamaa anajua kufunga kwa mashuti ya mbali makali ambayo yalimpa ubora mkubwa kwenye Ligi Kuu ya Zimbabwe na sasa anahamishia makali hayo Msimbazi.