Simba yashuka nafasi moja orodha ya klabu bora Afrika
Eric Buyanza
June 4, 2025
Share :
Klabu ya Simba SC imeshuka kwa nafasi moja katika orodha ya klabu bora Afrika kulingana na mafanikio yao kwenye Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Msimamo wa viwango vya klabu uliotolewa na CAF juzi kwa kupima mafanikio katika Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, Simba SC imeshika nafasi ya tano ikiwa na pointi 48 msimu huu kutoka nafasi ya nne kwa pointi 43 msimu uliopita.
Wekundu hao wa Msimbazi wamepinduliwa na RS Berkane iliyokuwa ya tano msimu wa 2023/24 kwa pointi 42 na kupaa hadi nafasi ya nne msimu huu kwa pointi.
Kinara ni Al Ahly ya Misri yenye pointi 78, Mamelodi Sundowns yenye pointi 62 imeshika nafasi ya pili, Esperance de Tunis ni ya tatu ikiwa na pointi 57 huku RS Berkane; mabingwa wapya wa Shirikisho Afrika wako nafasi ya nne wakiwa na pointi 52.
Katika msimamo huo, Yanga SC inashika nafasi ya 11 ikiwa na pointi 34, ikipanda kutoka nafasi ya 13 msimu uliopita kwa pointi 31.
Mafanikio hayo ya Simba SC yameifanya kuwa klabu ya kwanza kutoka Afrika Mashariki kufikia nafasi ya juu katika viwango vya Caf katika miaka ya hivi karibuni.
Msimamo huo ni kwa mujibu wa viwango vya CAF vinavyotolewa kwa kuzingatia matokeo ya klabu katika Mashindano yake kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.