Simbu aongoza mapambano dhidi ya Kisukari
Sisti Herman
August 17, 2026
Share :

Mwanariadha wa kimataifa wa Tanzania, Alphonce Simbu, ameibukia mapambano dhidi ya kisukari, akihamasisha Watanzania kufanya mazoezi mara kwa mara na kutumia zaidi vyakula vya asili kwa ajili ya afya zao.
Simbu ametoa kauli hiyo baada ya kutangazwa rasmi kuwa Balozi wa virutubisho vya Dhowbetic, vinavyolenga kusaidia watu wanaoishi na kisukari pamoja na wanaotaka kujikinga na ugonjwa huo.
Akizungumza baada ya uteuzi huo, Simbu amesema nidhamu ya maisha, ikiwamo kufanya mazoezi na kula vyakula vya asili, ni miongoni mwa mambo muhimu yanayoweza kusaidia katika mapambano dhidi ya kisukari.
“Kwenye michezo tunafundishwa sana kutumia vitu vya asili ili tuendelee kuimarika na kufanya vizuri. Maisha si mbio fupi, maisha ni marathon,” amesema Simbu.
Kauli hiyo inakuja wakati ugonjwa wa kisukari ukiendelea kuwa miongoni mwa changamoto za kiafya nchini, huku takwimu zilizotajwa kutoka Mfuko wa Taifa wa Taarifa za Afya kwa mwaka 2025 zikionyesha kuwa watu 863,741 wameathirika na ugonjwa huo nchini.





