Sistinho apewa tuzo kwa uchambuzi mahiri FIFA World Cup 2026
Sisti Herman
July 21, 2026
Share :

Mchambuzi wa soka Sisti Martin ‘Sistinho’ ametukiwa tuzo kwa uchambuzi mahiri alioufanya kwenye Kombe la dunia 2026 (FIFA World Cup 2026) kupitia shirika la habari Tanzania (TBC) ambapo alikuwa mmoja kati ya wachambuzi wa Televisheni ya TBC 1 waliokuwa na haki ya kuonyesha michuano hiyo na Radio ya TBC Taifa.
Tuzo hizo zimetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TBC Bi. Asha Dachi aliyeteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan wiki iliyopita kuchukua mikoba ya aliyekuwa Mkurugenzi mkuu wa Shirika hilo Bw. Ayoub Rioba Chacha.

Hafla ya kukabidhi zawadi hizo zimefanyika Julai 19, Makao makuu ya TBC, Mikocheni jijini Dar es salaam kabla mchezo wa fainali ya kombe la dunia kati ya Hispania dhidi ya Argentina ambapo Hispania waliibuka mabingwa wa dunia wakiifunga Argentina goli 1-0.
Sistinho, ambaye kwasasa ni mchambuzi wa PMTV Tanzania anasifika hasa kwa kufanya tathmini na uchambuzi wa kina wa kiufundi kuhusu mbinu za makocha wa timu mbalimbali (Tactical Analysis), takwimu za michezo (Stats & Data Analysis) na uchambuzi wa video (Video Analysis) na mambo mengine yanayohusiana zaidi na Sayansi ya mpira kupitia Makala anazoandika kupitia Tovuti ya PMTV Tanzania na Televisheni ya PMTV Tanzania, Jarida la Ligi Kuu 2025/26.
Kwa msimu huu uliotamatika hivi karibuni, Sistinho, amefanya tathmini za kina kwenye michuano mbalimbali kama Ligi Kuu Tanzania bara (NBC Premier League), Kombe la Shirikisho la TFF (CRDB Bank Federation Cup), Michuano ya Kombe la mataifa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN 2025), Michuano ya kombe la mataifa ya Afrika (AFCON 2025), Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League), Kombe la Mapinduzi (Mapinduzi Cup 2026) na Kombe la Muungano (Muungano Cup 2026).
Wasifu wa Sistinho na kazi zake kwa urefu unaweza kuuona kupitia ukurasa wake wa Instagram wa Sistiinho.





