Sitakubali vitisho kutoka popote, vikosi vya nyuklia viko macho – Vladmir Putin
Eric Buyanza
May 10, 2024
Share :
Rais Vladimir Putin wa Urusi amesisitiza kwamba nchi yake itafanya kila liwezekanalo ili dunia isitumbukie kwenye vita lakini amesema Urusi haitakubali vitisho kutoka upande wowote. Kauli hiyo ameitoa katika hotuba yake ya kuadhimisha "Siku ya Ushindi" wa umoja wa kisovieti dhidi ya manazi wa Ujerumani katika vita vikuu vya pili.
"Urusi itafanya kila linalowezekana kuzuia mzozo wa kimataifa. Lakini wakati huohuo hatutaruhusu mtu yeyote kututishia. Nguvu zetu za kimkakati ziko tayari kila wakati." Alisema Putin katika hotuba yake. Viongozi watano wa nchi zilizokuwa zamani kwenye umoja wa kisovieti walihudhuria sherehe hizo.
Viongozi hao ni kutoka nchi za Belarus, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Tajikistan na Turkmenistan.
Viongozi wengine washirika wa Urusi waliohudhuria ni kutoka Cuba, Laos na Guinea-Bissau. Hotuba ya Siku ya Ushindi ya Putin inatolewa wakati wanajeshi wake wanasonga mbele nchini Ukraine na mara tu baada ya kula kiapo cha kuongoza muhula wa tano madarakani. VOA