SMZ yapafunga New Amaan Complex kupisha maboresho ya AFCON 2027
Sisti Herman
August 17, 2026
Share :

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), imeufunga kwa muda Uwanja wa New Amaan Complex kwa ajili ya kurekebisha eneo la kuchezea kwa kupanda nyasi mpya.
Uamuzi wa kufanya hivyo ni kwa ajili ya kuandaliwa kutumika kwa mazoezi kuelekea Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) 2027.
Katika eneo la Uwanja wa New Amaan Complex, kuna viwanja vitatu ambapo viwili hutumika kwa ajili ya mazoezi, na mkubwa unaotumika kwa mechi za mashindano mbalimbali.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishna wa Idara ya Michezo Zanzibar, Ameir Moh’d Makame, wakati akitoa taarifa kuhusiana na maandalizi kuelekea AFCON 2027.
“Uwanja wa New Amaan Complex tumeufunga kwa muda kuimarisha nyasi kwa ajili ya mashindano ya AFCON, tutapanda mbegu mpya na mchakato huo utachukua miezi miwili kupanda, kuota na kuanza kukatwa,” amesema.





