Son aumizwa kushindwa kuisaidia Korea kusini dhidi ya Bafana Bafana
Eric Buyanza
June 25, 2026
Share :

Nahodha wa timu ya taifa ya Korea Kusini, Son Heung-min, ameanza mechi ya Kombe la Dunia akiwa benchi kwa mara ya kwanza tangu aanze kucheza soka la kimataifa mwaka 2010.
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Tottenham Hotspurs, alibaki benchi katika mchezo wa mwisho wa Kundi A dhidi ya South Africa uliochezwa kaskazini mashariki mwa Mexico.
Katika kipindi cha kwanza, Korea ilishindwa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga, hali iliyomfanya mchezaji huyo mkongwe kukiri baadaye kuwa alijihisi hana uwezo wa kusaidia timu akiwa nje ya uwanja.
Kocha wa Korea alimwingiza Son mwanzoni mwa kipindi cha pili wakati mchezo ukiwa bado suluhu, hata hivyo, Afrika Kusini ilifanikiwa kupata bao la ushindi katika dakika ya 63 na kulinda matokeo hayo hadi mwisho wa mchezo.
"Inasikitisha sana kwamba mechi haikuenda jinsi tulivyotaka, na sisi kama wachezaji ni wazi tumekatishwa tamaa sana," Son alisema. "Ninawahurumia wachezaji wenzangu kwamba sikuwapa msaada mkubwa uwanjani.”Alisema Son.
Ushindi huo wa bao 1-0 umeiwezesha Afrika Kusini kufuzu kwa mara ya kwanza katika historia yake kwenda hatua ya mtoano ya mashindano hayo.
Kwa upande wa Korea Kusini, matokeo hayo yameishusha hadi nafasi ya tatu katika Kundi A. Sasa timu hiyo italazimika kusubiri matokeo ya mechi zilizobaki za hatua ya makundi ili kubaini kama itakuwa miongoni mwa timu nane bora zilizomaliza katika nafasi ya tatu na hivyo kupata tiketi ya kwenda hatua ya mtoano.





