Spika wa Uganda amuita Museveni 'Mungu' na mtoto wake 'Mwana wa Mungu'
Eric Buyanza
June 10, 2025
Share :
Watu mbalimbali katika mitandao ya kijamii wametoa maoni yao kumlaani Spika wa Bunge la Uganda baada ya kusema kuwa Rais Yoweri Museveni ni Mungu na kumwita mwanae Mwana wa Mungu.
Akiwa Kyazanga, kilomita 50 kusini mwa mji wa Masaka, Spika Anita Among alipiga magoti na kuwaomba watu wa eneo hilo kuwapigia kura wabunge wa chama cha NRM aliowateua, akisema: "Napiga magoti, namuunga mkono Rais Museveni" na wagombea wa NRM. Kisha akasimama.
Katika video hiyo iliyowekwa kwenye mitandao ya kijamii, Anita aliongeza: "Kama nilivyowaambia mara ya mwisho, sisi katika Teso [eneo lililo mashariki mwa Uganda] tunaamini Utatu Mtakatifu. Tunaamini katika Mungu Baba, na Mungu Baba ni Rais Museveni, [anarudia] Mungu Baba ni Rais Museveni. Mungu Mwana ni MK [Muhoozi Kainerugaba], sasa nyinyi mko katika Roho Mtakatifu, kwa hiyo muwachague.
Gazeti la Daily Monitor la Uganda limeripoti kuwa kumuita Rais Museveni kuwa Mungu kumewakasirisha baadhi ya viongozi wa kidini wanaosema ni kufuru.
Bunge la Uganda limejibu kwa kusema matamshi ya Anita yalikuwa 'mfano tu'.