pmbet

Spurs yasalimu amri kwa mashabiki, yarudisha jina la "Tottenham"

Eric Buyanza

October 12, 2026
Share :

Klabu ya soka ya Tottenham Hotspur imelazimika kusalimu amri na kufanya mageuzi makubwa ya maamuzi (U-turn) baada ya mpango wao wa kupiga marufuku jina la "Tottenham" kukataliwa katakata na mashabiki wa timu hiyo.

 

Sakata hili lilianza kushika kasi mnamo Novemba 2024 wakati klabu hiyo ilipozindua muonekano na utambulisho mpya wa chapa yao (brand identity). Mambo yalikuja kuwa moto zaidi mnamo Februari 2025, pale uongozi wa Spurs ulipotuma barua pepe rasmi kwa uongozi wa Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League) na vyombo vya habari, ukitaka watangazaji waache mara moja kuliita klabu hiyo jina la "Tottenham" pekee.

 

Viongozi wa klabu hiyo walisisitiza kuwa jina "Tottenham" linawakilisha eneo la kijiografia la Kaskazini mwa London na sio klabu yenyewe, hivyo walitaka timu hiyo iitwe tu "Tottenham Hotspur" au "Spurs."

 

Hatua hiyo ilionekana kama "kituko cha karne" na iliwakasirisha mno mashabiki wa jadi wa timu hiyo. Mashabiki walilalamika kuwa klabu hiyo inajaribu kufuta historia, utamaduni, na mizizi ya timu ambayo imekuwepo kwa miongo mingi, ambapo neno "Tottenham" limekuwa likitumika kwenye nyimbo na kauli mbiu zao za kila siku.

 

Baada ya shinikizo kubwa na vikao vizito kati ya viongozi wa klabu na Bodi ya Ushauri ya Mashabiki, hatimaye uongozi wa Spurs umekubali yaishe na kugeuza msimamo wao.

 

Kwa sasa, klabu imerejesha rasmi matumizi ya jina hilo uwanjani. Kauli mbiu maarufu ya "This is Tottenham" sasa inang'ara tena kwenye skrini kubwa za uwanja wa Tottenham Hotspur Stadium na kwenye mabango ya kidijitali kabla ya mechi kuanza, kuashiria ushindi mkubwa kwa sauti ya mashabiki dhidi ya maamuzi ya kibiashara ya bodi.

pmbet
pmbet

Leagues standings

Tanzania Premier League
pmbet
pmbet