Taasisi feki yaanzishwa ndani ya ofisi ya Rais na kujilipa Bilioni 2
Eric Buyanza
July 9, 2026
Share :

Rais wa Nigeria, Bola Tinubu, ameagiza kufanyika kwa uchunguzi wa tuhuma za ufisadi baada ya madai kwamba taasisi ya serikali isiyokuwepo kisheria iliundwa ndani ya ofisi yake na kupewa fedha za umma zenye thamani ya dola za Marekani 950,000 (Bilioni 2.4 kitanzania).
Kwa mujibu wa Ikulu ya Nigeria, barua iliyodaiwa kutolewa na Mkuu wa Wafanyakazi wa Rais ya kuanzisha Presidential Foreign Intervention Promotion Council (PFIPC) ilikuwa ya kughushi.
Polisi wameanzisha msako dhidi ya Adeniyi Adeyemi Matthew, ambaye alikuwa akijitambulisha kama Mkurugenzi Mkuu wa PFIPC, kwa tuhuma za kughushi nyaraka, kujifanya afisa wa umma na makosa mengine yanayohusiana.
Kabla ya kutoweka, Adeyemi aliviambia vyombo vya habari vya nchini humo kuwa hana hatia na kwamba ana hofu kuhusu usalama wa maisha yake.
Aliahidi kufika mahakamani kuthibitisha kutokuwa na hatia, akisisitiza kuwa taasisi hiyo ilianzishwa kwa mujibu wa sheria. Pia aliwashutumu baadhi ya maafisa waandamizi serikalini kwa kudai rushwa wakati wa mchakato wa uteuzi wake na baadaye kujaribu kudhibiti fedha za taasisi hiyo. Ikulu imekanusha tuhuma hizo.
Adeyemi alisema PFIPC ilianzishwa mwaka 2024 kwa lengo la kuvutia uwekezaji wa kigeni nchini Nigeria, lakini hakuna rekodi yoyote inayoonesha kuwa ilifanikiwa kufanikisha uwekezaji wowote.
Taasisi hiyo ina wafanyakazi watatu pekee, ambao tayari wamehojiwa na polisi.
Jumanne, Rais Tinubu aliiagiza Tume Huru ya kupambana na vitendo vya rushwa (ICPC) kufanya uchunguzi na kuwasilisha ripoti kamili ndani ya siku 30.
BBC





