Tabora wajichimbia Shinyanga wakiwasubiri Simba
Sisti Herman
January 17, 2024
Share :
Timu ya Tabora United imeingia kambini leo mkoani Shinyanga kwa ajili ya kuanza maandalizi ya michezo ya Ligi Kuu ya NBC Soka Tanzania bara pamoja na michuano ya kombe la Azam Sport Federation (ASFC).
Tabora United chini ya kocha Mkuu Goran Copunovic imeweka kambi ya wiki mbili mkoani humo ambapo itakuwa ikijifua wakati huu ambao Ligi Kuu imesimama kupisha michuano ya kombe la Mataifa Afrika (AFCON) inayoendelea Nchini Ivory Coast.
“Aidha wachezaji wote wameingia kambini wakiwa na Afya nzuri ,hari na morali ya kutumia mapumziko haya kwa ajili ya kufanya maandalizi kulingana na program za kocha Kopunovic ikiwemo kufanya mazoezi ya uwanjani pamoja na kucheza mechi za kirafiki ili kuwajenga kutokana na kuwa nje kwa kipindi kirefu bila mchezo wowote wakimashindano”.
“ Tumeingia leo hapa Shinyanga kwa ajili ya kuweka kambi ya kujiandaa na michezo yetu ya Ligi Kuu pamoja na michuano ya Kombe la ASFC, tunamshukuru Mungu wachezaji wetu wote wamerejea salama hakuna mwenye changamoto yoyote na kila mmoja yupo tayari kuhakikisha kwamba wanatumia vizuri kipindi hiki cha maandalizi ya michezo yetu'.
"Mara nyingi inapotokea mapumziko ya muda mrefu kama hivi sasa, nilazima Timu iwe na mipango mikakati ya kulinda viwango vya wachezaji kwa maana Ligi ni ngumu hata ukiangalia kwenye msimamo Timu nyingi zinakimbizana hivyo kuanza mapema kambi ni moja ya mikakati ya kuwaweka vizuri wachezaji wetu”. ilieleza sehemu ya taarifa kwa umma kutoka idara ya habari ya timu hiyo.
Tabora United kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ipo kwenye nafasi ya 12 ikiwa imecheza jumla ya mechi 13 ambapo kwenye mchezo wa mwisho ilipoteza dhidi ya Yanga katika uwanja wa Jamuhuri Dodoma kwa goli 1-0.
Hata hivyo Tabora United imebakiza michezo miwili ili kukamilisha mzunguko wa kwanza ambapo michezo hiyo ni dhidi ya Namungo pamoja na Simba na kwamba yote itapigwa katika uwanja wa Alhasan Mwinyi mara tu Ligi itakaporejea.