Tanzania yaambulia sare kwa Zambia Afcon
Sisti Herman
January 21, 2024
Share :
Sare ya bao 1-1 dhidi ya Zambia leo kwenye fainali za mataifa ya Afrika, imeipa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' pointi ya kwanza ambayo imeifanya kuwa na nafasi ya kufuzu hatua ya 16 bora kulingana na msimamo wa kundi F ulivyo.
Ingawa Taifa Stars inashika mkia katika kundi hilo na pointi yake moja, inaweza kufuzu hatua ya 16 bora ikiwa itaibuka na ushindi katika mechi ya mwisho dhidi ya DR Congo na Zambia ikashindwa kupata ushindi dhidi ya Morocco.
Lakini hata Zambia ikishinda, Taifa Stars inaweza kufuzu ikiwa itaifunga DR Congo kupitia nafasi nne zinazotolewa kwa timu zilizoshika nafasi ya tatu zikiwa na matokeo bora kwenye makundi.
Katika mechi ya leo, Taifa Stars ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Saimon Msuva katika dakika ya 12 kabla ya patson Daka kuisawazishia Zambia katika dakika ya 88.
Kwa sasa Morocco inaongoza kundi F ikiwa na pointi nne, ikifuatiwa na DR Congo na Zambia ambazo kila moja ina pointi mbili na Taifa Stars iko mkiani ikiwa na pointi moja.