Tanzania yazindua chumba cha ufuatiliaji maafa cha kwanza Afrika
Eric Buyanza
June 15, 2024
Share :
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) imezinduzi Chumba maalum cha Ufuatiliaji wa Mwenendo wa Majanga na Tahadhari ya Mapema (Situation Room for Mult-Hazard Monitoring and Early Warning) katika Kituo cha Taifa cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura kilichopo Jijini Dodoma, Mji wa Serikali Mtumba.
Uanzishaji wa chumba hicho utaimarisha upatikanaji wa taarifa za uwezekano wa kutokea kwa majanga na tahadhari za mapema kwa wanajamii wote na taasisi mbalimbali na hivyo kuwezesha kuzuia au kupunguza madhara ya majanga.
Akizungumza kwenye uzinduzi huo leo June 14,2024 Jijini Dodoma,Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Jenista Joakim Mhagama amesema humba hicho kimeanzishwa ikiwa ni sehemu ya Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura na kutarajiwa kuimarisha operesheni za majanga kwa kuunganisha vituo mbalimbali vya kisekta, Kituo cha kikanda vya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika, Kituo cha Jumuiya ya Afrika Mashariki na Kituo cha Kamisheni ya Umoja wa Afrika.
“Chumba hiki kimefungwa vifaa mbalimbali vya TEHAMA pamoja na mifumo mbalimbali ya kufuatilia mwenendo wa majanga na tahadhari ya mapema ikijumuisha jukwaa la ki-eletroniki la myDEWETRA ambalo limeunganisha taarifa za kijiografia kwa ajili ya uchambuzi wa utabiri wa hali ya hewa na haidrolojia hatarishi ya mafuriko, ukame, vimbunga, Tsunami na upepo mkali ili kuweza kufanya tathmini ya madhara na kutoa tahadhari ya mapema kwa wakati na eneo husika,”ameeleza.
Mhagama pia ametumia nafasi hiyo kutoa wito kwa wataalam wote watakaopangiwa kufanya kazi katika chumba hicho kuhakikisha kuwa shughuli zilizopangwa kufanyika zinatekelezwa kwa ufanisi ili kuhakikisha taarifa za tahadhari za mapema zinawafikia walengwa kwa wakati hasa wanajamii na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kuchukua hatua za haraka za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga.