pmbet

Tathmini ya Pawasa Simba vs Ahly "Wanahitaji zaidi akili ya Chama kuliko mwili"

Sisti Herman

March 29, 2024
Share :

Kuelekea mchezo wa robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika kati ya wenyeji klabu ya Simba dhidi ya wageni kutoka Misri klabu ya Al Ahly, PM SPORTS imeungana na aliyekuwa mchezaji mwandamizi wa Simba na Taifa Stars ambaye kwasasa ni kocha wa timu ya Taifa ya soka la ufukweni Bonophace Pawasa kukuletea tathmini ya mchezo huu kupitia mahojiano ya maalumu na mwandishi wa makala haya.

 

Kama Kocha kipi ungesisitiza kwa wachezaji kuelekea mchezo kabla ya Mbinu?

 

“Ningewasisitiza kuwa tunapaswa kumaliza mechi nyumbani kwa kushinda idadi kubwa ya mabao ili kurahisisha mazingira ya kufuzu ugenini kwa kutumia vyema nafasi chache tutakazotengeneza kwasababu mechi za ugenini hasa Afrika kaskazini huwa zinaamuliwa na mambo mengi sana kabla ya mbinu na ufundi”

 

“Mechi za mtoano faida kubwa ni kuutumia uwanja wa nyumbani, tuwatumie vizuri mashabiki wa kwa mkapa”

 

Ni eneo kimbinu huwafanya Al Ahly kuwa bora zaidi uwanjani?

 

“Ubora wa Al Ahly ugenini huwa kwenye nyakati za kutegea, hawatumii nishati kubwa, huwa wanatumia mfumo wa 4-3-3 lakini wasipokuwa na mpira huwa watano katikati, 4-5-1, wale mawinga wao (El Shehat na Percy Tau) huwa sambamba na viungo wa kati katikati ya uwanja (Mid Block) nyakati za kuzuia wakisubiri mashambulizi ya kushtukiza”

 

“Mashambulizi yao ya kushtukiza huwategemea zaidi mawinga, hasa Percy Tau, wana kasi sana na uwezo wa mmoja dhidi ya mmoja kushambulia kwenye mapana ya uwanja kisha kuanza kulitafuta boksi la wapinzani”

 

“Ubora pia unaanzia kwa viungo wa kati na pembeni, hasa yule aliyemuia juzi (Emam Ashour), huwa wanatumia viungo watatu wa kati, wawili chini na mmoja mbele yao, huyo wa mbele yao huwa anakuwa huru sana na kwenye mashambulizi ya kushtukiza wale wengine huwa haraka sana kupiga pasi kwenye maeneo”

 

“Watu hudhani Al Ahly wamechoka, siyo kweli, wamefika hatua hii kama wanavyofikaga siku zote, mkiwa wazembe uwanjani kucheza kama timu ubora wa wachezaji wao unaweza kuwaua, wana wachezaji wenye uwezo na viwango vikubwa kuliko wa Simba”

 

Simba wana wastani wa kuruhusu kila mchezo wanaocheza, wanapaswa kuwazuia vipi Al Ahly?

 

“Wakicheza kama walivyocheza dhidi ya Asec Mimosas ugenini wataweza kuwazuia vizuri, walizuia na mfumo wa 4-1-4-1, wachezaji wa mbele hawakutegea kuzuia, mara nyingi hili ndiyo tatizo la Simba, wanapaswa kuzuia kwa muundo na mbinu kama zile Mshambuliaji asiruhusu mabeki wa Al Ahly wawe huru, ahakikishe anawapa presha, viungo wanne nyuma yake wahakikishe wawili hawawaruhusu viungo wa kati wa Ahly kupokea pasi kutoka kwa mabeki na kupeleka mbele, hapa huwa namuona Kanoute akizuia vizuri”

 

“Lakini pia mawinga wasiruhusu wale mabeki wawili wa pembeni wa Ahly wawe huru, wawape presha Al Maaloul na Mohamed Hany, wakizuia hivi watawapokonya mipira kujibu mashambulizi lakini pia wakipitwa wakimbie sana uwanjani kwani bila kufanya hivyo wenzao wa nyuma watakuwa hatarini, kwa pembeni mfano mzuri wa namna ya kuzuia ni ile kasi, nishati na nidhamu ya Kibu, pande zote wacheze hivyo”

 

Unadhani mchezaji gani wa Simba anaweza kubeba timu?

 

“Nyota wa Simba ni Chama, na leo Simba inahitaji zaidi akili yake kuliko mwili, maamuzi yake sahihi kwenye eneo la wapinzani yaliamua mechi kubwa nyingi hivyo hata ya leo pia nampa nafasi hiyo, leo ndo anapaswa kutuonyesha ule ukubwa wake, ukubwa huonyeshwa kwenye nyakati kubwa”

 

“Lakini mechi kubwa hazipaswi kumtegemea mchezaji mmoja, wacheze kama timu, kila mmoja atimize majukumu yake kwa usahihi na ufasaha”

 

Tahadhari zipi Simba wazichukue kwenye mchezo kwa uzoefu wako dhidi ya timu za Afrika kaskazini?

 

“Timu za Afrika kaskazini zina mbinu nyingi hasa za kisaikolojia kuwadanganya waamuzi kwa kujiangusha na kulalamika ili mpate kadi na kumbuka ukipata kadi unapunguziwa kasi ya kuzuia kama wewe ni beki kwasababu unaogopa kupata nyingine”

 

“Lakini pia waarabu wanagawa mechi kwenye nyakati nne za vipindi viwili, dakika 15 za mwanzo watakupa presha kubwa ili wapate goli baada ya hapo wanasubiri nyuma hadi kipindi cha kwanza kiishe, wakirejea tena wanakupa presha kwa dakika 10 za mwanzo kipindi cha pili baada ya hapo wanasubiri dakika 10 za mwisho wakupe tena presha wanaamini hizo ni nyakati ambazo nyie mnakuwa hampo mchezoni kiakili”

 

Simba ina wastani wakuruhusu kwa kutumia mipira ya kutenga, tahadhari ipi unawapa?

 

“Wachezaji wanapswa kuwa makini sana na kona na faulo, hasa nyakati za kuzuia, waarabu wanafunga sana aina hiyo ya mabao, wanapaswa kuwasiliana sana, kushinda kila kitu uwanjani, kuruka, kushinda mipira juu na inayozagaa zagaa kufanya hivyo wataweza kuzuia vizuri aina hiyo ya mabao”

 

Simba washinde kwaajili ya Christopha Alex na Ramadhan Wasso na mashabiki waliopata ajali leo

 

“Miaka 20 iliyopita kwenye ile timu yetu iliyowatoa Zamalek ugenini Misri, wawili kati yetu wamefariki, Christopher Alex na Ramadhan Wasso, hvyo natamani kuona kila mchezaji wa Simba akipambana kukumbuka namna watu hao walivyotoa jasho lao kwa Simba”

 

“Lakini pia wachezaji wa Simba washinde kwaajili ya mashabiki waliopata ajali wakiwa safarini kuja, mpira ni kwaajili ya mashabiki”

 

Alihitimisha hivyo Pawasa kutoa tathmini yake kuelekea mchezo huo leo.

pmbet
pmbet

Leagues standings

Tanzania Premier League
pmbet
pmbet